Psalms 12

Kuomba Msaada

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Sheminithi: Zaburi Ya Daudi)

BWANA tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka;
waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.
Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;
midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.
BWANA na akatilie mbali midomo yote ya hila
na kila ulimi uliojaa majivuno
ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;
midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”
“Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge
na kulia kwa uchungu kwa wahitaji,
nitainuka sasa,” asema BWANA.
“Nitawalinda kutokana na wale
wenye nia mbaya juu yao.”
Maneno ya BWANA ni safi,
kama fedha iliyosafishwa katika tanuru,
iliyosafishwa mara saba.
Ee BWANA, utatuweka salama
na kutulinda na kizazi hiki milele.
Watu waovu huenda wakiringa kila mahali
wakati ambapo yule aliye mbaya sana
ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.
Copyright information for Neno