Psalms 135

Wimbo Wa Sifa Kwa Mungu

Msifuni BWANA.
Lisifuni jina la BWANA,
msifuni, enyi watumishi wa BWANA,
ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya BWANA,
katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
Msifuni BWANA, kwa kuwa BWANA ni mwema,
liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.
Kwa maana BWANA amemchagua Yakobo
kuwa wake mwenyewe,
Israeli kuwa mali yake ya thamani.
Ninajua ya kuwa BWANA ni mkuu,
kwamba Bwana wetu ni mkuu zaidi
kuliko miungu yote.
BWANA hufanya lo lote apendalo,
mbinguni na duniani,
katika bahari na vilindi vyake vyote.
Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia;
hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua
na huleta upepo kutoka ghala zake.
Alimwua mzaliwa wa kwanza wa Misri,
mzaliwa wa kwanza
wa wanadamu na wanyama.
Alipeleka ishara zake na maajabu
katikati yako, Ee Misri,
dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
10 Aliyapiga mataifa mengi,
na akaua wafalme wenye nguvu:
11 Mfalme Sihoni na Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani
na wafalme wote wa Kanaani;
12 akatoa nchi yao kuwa urithi,
urithi kwa watu wake Israeli.
13 Ee BWANA, jina lako ladumu milele,
kumbukumbu za fahari zako,
Ee BWANA, kwa vizazi vyote.
14 Maana BWANA atawathibitisha watu wake
kuwa wenye haki,
na kuwahurumia watumishi wake.
15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona,
17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.
18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wote wanaozitumainia.
19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni BWANA;
Ee nyumba ya Aroni, msifuni BWANA;
20 Ee nyumba ya Lawi, msifuni BWANA;
ninyi mnaomcha, msifuni BWANA.
21 Msifuni BWANA kutoka Sayuni,
msifuni yeye aishiye Yerusalemu.
Msifuni BWANA.
Copyright information for Neno