Psalms 137

Maombolezo Ya Israeli Uhamishoni

Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza
tulipokumbuka Sayuni.
Kwenye miti ya huko
tulitundika vinubi vyetu,
kwa maana huko hao waliotuteka
walitaka tuwaimbie nyimbo,
watesi wetu walidai nyimbo za furaha;
walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja
kati ya nyimbo za Sayuni!”
Tutaimbaje nyimbo za BWANA,
tukiwa katika nchi ya kigeni?
Nikikusahau wewe, Ee Yerusalemu,
basi mkono wangu wa kuume
na usahau ujuzi wake.
Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu
kama sitakukumbuka wewe,
kama nisipokufikiri Yerusalemu
kuwa furaha yangu kubwa.
Kumbuka, Ee BWANA,
walichokifanya Waedomu,
siku ile Yerusalemu ilipoanguka.
Walisema, “Bomoa, Bomoa
mpaka kwenye misingi yake!”
Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa,
ana furaha yeye ambaye atakulipiza wewe
kwa yale uliyotutenda sisi:
yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga
na kuwaponda juu ya miamba.
Copyright information for Neno