Psalms 138

Maombi Ya Shukrani

(Zaburi Ya Daudi)

Nitakusifu wewe, Ee BWANA,
kwa moyo wangu wote,
mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.
Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,
nami nitalisifu jina lako
kwa ajili ya upendo wako
na uaminifu,
kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako
juu ya vitu vyote.
Nilipoita, ulinijibu;
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
Wafalme wote wa dunia,
na wakusifu wewe Ee BWANA,
wakati wanaposikia
maneno ya kinywa chako.
Wao na waimbe kuhusu njia za BWANA,
kwa maana utukufu wa BWANA ni mkuu.
Ingawa BWANA yuko juu,
humwangalia mnyonge,
bali mwenye kiburi
yeye anamjua kutokea mbali.
Nijapopita katikati ya shida,
wewe unayahifadhi maisha yangu,
unanyosha mkono wako
dhidi ya hasira ya adui zangu,
kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.
BWANA atatimiza kusudi lake kwangu,
Ee BWANA, upendo wako wadumu milele:
usiziache kazi za mikono yako.
Copyright information for Neno