Psalms 142

Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Watesi

(Utenzi Wa Daudi Alipokuwa Pangoni. Maombi)

Namlilia BWANA kwa sauti kubwa,
nainua sauti yangu kwa BWANA anihurumie.
Namimina malalamiko yangu mbele zake,
mbele zake naeleza shida zangu.
Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu,
wewe ndiwe unajua njia zangu.
Katika njia ninayopita
watu wameweka mtego
kwa ajili yangu.
Tazama kuume kwangu na uone,
hakuna hata mmoja anayejihusisha nami.
Sina kimbilio,
hakuna anayejali maisha yangu.
Ee BWANA, nakulilia wewe,
nasema, “Wewe ni kimbilio langu,
fungu langu katika nchi ya walio hai.”
Sikiliza kilio changu,
kwa sababu mimi ni mhitaji sana;
niokoe na wale wanaonifuatilia,
kwa kuwa wamenizidi nguvu.
Nifungue kutoka katika kifungo changu,
ili niweze kulisifu jina lako.
Ndipo wenye haki watanizunguka,
kwa sababu ya wema wako kwangu.
Copyright information for Neno