Psalms 16

Sala ya Matumaini

(Utenzi wa Daudi)

Ee Mungu, uniweke salama,
kwa maana kwako nimekimbilia.
Nilimwambia BWANA, “Wewe ndiwe Bwana wangu;
pasipo wewe sina jambo jema.”
Kwa habari ya watakatifu walioko duniani,
ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao.
Huzuni itaongezeka kwa wale
wanaokimbilia miungu mingine.
Sitazimimina sadaka zao za damu
au kutaja majina yao midomoni mwangu.
BWANA umeniwekea fungu langu na kikombe changu;
umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.
Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,
hakika nimepata urithi mzuri.
Nitamsifu BWANA ambaye hunishauri,
hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.
Nimemweka BWANA mbele yangu daima.
Kwa kuwa yupo mkono wangu wa kuume,
sitatikiswa.
Kwa hiyo moyo wangu una furaha na ulimi wangu unashangilia;
pia mwili wangu utapumzika salama,
10 kwa sababu hutanitelekeza kuzimu,
wala hutaacha Mtakatifu Wako aone uharibifu.
11 Umenijulisha njia ya uzima;
utanijaza na shangwe katika uwepo wako,
pamoja na furaha za milele
katika mkono wako wa kuume.
Copyright information for Neno