Psalms 18

Wimbo Wa Daudi Wa Ushindi

(2 Sam 22:1-15)

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Mtumishi Wa Mungu Aliyomwimbia Mungu Wakati Mungu Alipomwokoa Mkononi Mwa Sauli Na Adui Wengine)

1Nakupenda wewe, Ee BWANA,
nguvu yangu.
2BWANA ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
Mungu wangu ni mwamba,
ambaye kwake ninakimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,
ngome yangu.
3Ninamwita BWANA anayestahili kusifiwa,
nami nimeokoka kutoka kwa adui zangu.
4Kamba za mauti zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
5Kamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
6Katika shida yangu nalimwita BWANA,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika mbele zake,
masikioni mwake.
7Dunia ikatetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikayumbayumba,
ilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.
8Pua zake zilitoa moshi,
moto uteketezao ulitoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo
yakatoka ndani mwake.
9Alizipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
10Alipanda kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.
11Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika,
chandarua chake kumzunguka,
mawingu meusi ya mvua angani.
12Kutokana na mwanga mkali wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.
13BWANA alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
14Aliipiga mishale yake na kutawanya adui,
naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.
15Ee BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako,
sakafu ya bahari ikaonekana,
misingi ya dunia ikawa wazi.
16Akanyosha mkono wake kutoka juu, akanishika,
akanitoa kutoka katika maji mengi.
17Akaniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu,
waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
18Walinishambulia siku ya taabu yangu,
lakini BWANA alikuwa msaada wangu.
19Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
20BWANA alinitendea sawa sawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
21Kwa maana nimezishika njia za BWANA,
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
22Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
23Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
24BWANA amenilipa sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.
25Kwa yeye aliye mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionyesha kutokuwa na hatia.
26Kwa aliye safi unajionyesha kuwa safi,
lakini kwa aliyepotoka unajionyesha kuwa mkaidi.
27Wewe huwaokoa wanyenyekevu
lakini huwashusha wenye kiburi.
28Wewe, Ee BWANA, unaifanya taa yangu
iendelee kuwaka,
Mungu wangu hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
29Kwa msaada wako nitashinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
30Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,
neno la BWANA ni kamili.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
31Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya BWANA?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
32Mungu ndiye anivikaye nguvu na
kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
33Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
34Huifundisha mikono yangu kupigana vita,
mikono yangu inaweza
kupinda upinde wa shaba.
35Hunipa ngao yako ya ushindi,
mkono wako wa kuume hunitegemeza,
huinama chini ili kuniinua.
36Hupanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
37Niliwafuatia adui zangu na nikawapata,
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
38Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena,
walianguka chini ya miguu yangu.
39Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita,
adui zangu uliwafanya wasujudu miguuni pangu.
40Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
41Walipiga yowe kuomba msaada,
lakini hapakuwepo na ye yote wa kuwaokoa;
walimlilia BWANA, lakini hakuwajibu.
42Niliwaponda wakawa kama mavumbi
yanayopeperushwa na upepo,
nikawamwaga nje kama tope barabarani.
43Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu;
umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa,
watu ambao sikuwajua wananitumikia.
44Mara wanisikiapo hunitii,
wageni hunyenyekea mbele yangu.
45Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
46BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!
47Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
awatiishaye mataifa chini yangu,
48aniokoaye na adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka watu wajeuri.
49Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee BWANA;
nitaliimbia sifa jina lako.
50Humpa mfalme wake ushindi mkuu,
huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na uzao wake milele.
Copyright information for Neno