Psalms 27

Sala Ya Kusifu

(Zaburi Ya Daudi)

BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu,
nimwogope nani?
BWANA ni ngome ya uzima wangu,
nimhofu nani?
Waovu watakaposogea dhidi yangu
ili waile nyama yangu,
adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,
watajikwaa na kuanguka.
Hata jeshi linizunguke pande zote,
moyo wangu hautaogopa;
hata vita vitokee dhidi yangu,
hata hapo nitakuwa na ujasiri.
Jambo moja ninamwomba BWANA,
hili ndilo ninalolitafuta:
niweze kukaa nyumbani mwa BWANA
siku zote za maisha yangu,
niutazame uzuri wa BWANA
na kumtafuta hekaluni mwake.
Kwa kuwa siku ya shida,
atanihifadhi salama maskani mwake,
atanificha uvulini mwa hema yake
na kuniweka juu kwenye mwamba.
Kisha kichwa changu kitainuliwa
juu ya adui zangu wanaonizunguka;
katika maskani yake nitatoa dhabihu
kwa kelele za shangwe;
nitamwimbia BWANA na kumsifu.
Uisikie sauti yangu nikuitapo, Ee BWANA,
unihurumie na unijibu.
Moyo wangu unasema kuhusu wewe,
“Utafute uso wake!”
Uso wako, BWANA “Nitautafuta.”
Usinifiche uso wako,
usimkatae mtumishi wako kwa hasira;
wewe umekuwa msaada wangu.
Usinikatae wala usiniache,
Ee Mungu Mwokozi wangu.
10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,
BWANA atanipokea.
11 Nifundishe njia yako, Ee BWANA,
niongoze katika njia iliyonyooka
kwa sababu ya watesi wangu.
12 Usinitie katika nia ya adui zangu,
kwa maana mashahidi wa uongo
wameinuka dhidi yangu,
wakipumua jeuri.
13 Nami bado nina tumaini hili:
nitauona wema wa BWANA
katika nchi ya walio hai.
14 Umngojee BWANA,
uwe hodari na mwenye moyo mkuu,
nawe, umngojee BWANA.
Copyright information for Neno