Psalms 28

Kuomba Msaada

(Zaburi Ya Daudi)

Ninakuita wewe, Ee BWANA, Mwamba wangu;
usiwe kwangu kama kiziwi.
Kwa sababu ukinyamaza
nitafanana na hao
waliokwisha shuka shimoni.
Sikia kilio changu unihurumie
ninapokuita kwa ajili ya msaada,
niinuapo mikono yangu kuelekea
Patakatifu pa Patakatifu pako.
Usiniburute pamoja na waovu,
pamoja na hao watendao mabaya,
ambao huzungumza na jirani zao
maneno mazuri,
lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
Uwalipe sawasawa na matendo yao,
sawasawa na matendo yao maovu;
walipe sawasawa na kazi za mikono yao,
uwalipe wanavyostahili.
Kwa kuwa hawaheshimu kazi za BWANA,
na yale ambayo mikono yake imetenda,
atawabomoa na kamwe
hatawajenga tena.
BWANA asifiwe,
kwa maana amesikia kilio changu
nikimwomba anihurumie.
BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
BWANA ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
Waokoe watu wako na uubariki urithi wako;
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.
Copyright information for Neno