Psalms 33

Ukuu Na Wema Wa Mungu

1Mwimbieni BWANA kwa furaha, enyi wenye haki;
kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
2Msifuni BWANA kwa kinubi,
mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
3Mwimbieni wimbo mpya;
pigeni kwa ustadi,
pigeni kelele za furaha.
4Maana neno la BWANA ni haki na kweli,
ni mwaminifu kwa yote atendayo.
5Hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani
kwa pumzi ya kinywa chake.
7Ameyakusanya maji ya bahari
kama kwenye mtungi;
vilindi vya bahari
ameviweka katika ghala.
8Dunia yote na imwogope BWANA,
watu wote wa dunia wamche.
9Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
10BWANA huzuia mipango ya mataifa,
hupinga makusudi ya mataifa.
11Lakini mipango ya BWANA
inasimama imara milele,
makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
12Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao,
watu ambao aliwachagua
kuwa urithi wake.
13Kutoka mbinguni BWANA hutazama chini
na kuwaona wanadamu wote;
14kutoka maskani mwake huwaangalia
wote wakaao duniani,
15yeye ambaye huumba mioyo yao wote,
ambaye huangalia
kila kitu wanachokitenda.
16Hakuna mfalme aokokaye
kwa ukubwa wa jeshi lake;
hakuna shujaa aokokaye
kwa wingi wa nguvu zake.
17Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu,
licha ya nguvu zake nyingi hawezi kuokoa.
18Lakini macho ya BWANA yako kwa wale wamchao,
kwa wale ambao tumaini lao
ni katika upendo wake usio na kikomo,
19ili awaokoe na mauti,
na kuwahifadhi wakati wa njaa.
20Sisi tunamngojea BWANA kwa matumaini,
yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21Katika yeye mioyo yetu hushangilia,
kwa maana tunalitumainia
jina lake takatifu.
22Upendo wako usio na mwisho
ukae juu yetu, Ee BWANA,
kama vile tunavyoweka
tumaini letu kwako.
Copyright information for Neno