Psalms 34

34:0 Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22

Sifa Na Wema Wa Mungu

(Zaburi Ya Daudi, Alipojifanya Mwendawazimu Mbele Ya Abimeleki, Ambaye Alimfukuza, Naye Akaondoka)

Nitamtukuza BWANA nyakati zote,
sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote.
Nafsi yangu itajisifu katika BWANA
walioonewa wasikie na wafurahi.
Mtukuzeni BWANA pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
Nilimtafuta BWANA naye akanijibu,
akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
Wale wamtazamao hutiwa nuru,
nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
Maskini huyu alimwita BWANA akamsikia,
akamwokoa katika taabu zake zote.
Malaika wa BWANA hufanya kituo
akiwazunguka wale wamchao,
naye huwaokoa.
Onjeni mwone kwamba BWANA ni mwema,
heri mtu yule anayemkimbilia.
Mcheni BWANA enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na kitu cho chote.
10 Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wamtafutao BWANA
hawatakosa kitu cho chote kilicho chema.
11 Njoni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha BWANA.
12 Ye yote kati yenu anayependa maisha
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13 auzuie ulimi wake na mabaya
na midomo yake kutokana
na kusema uongo.
14 Aache uovu na atende mema,
aitafute amani na kuifuatia.
15 Macho ya BWANA yako kwa wenye haki
na masikio yake yako makini
kusikia kilio chao;
16 uso wa BWANA uko kinyume na watenda mabaya,
kufuta kumbukumbu lao duniani.
17 Wenye haki hulia, naye BWANA huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18 BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo
na huwaokoa waliopondeka roho.
19 Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini BWANA humwokoa nayo yote,
20 huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21 Ubaya utamwua mtu mwovu,
adui za mwenye haki watahukumiwa.
22 BWANA huwakomboa watumishi wake,
wale wanaomkimbilia yeye
hawatahukumiwa hata mmoja wao.
Copyright information for Neno