Psalms 36

Uovu Wa Mwanadamu

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Mtumishi Wa Mungu)

Kuna neno moyoni mwangu
kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.
Hakuna hofu ya Mungu
mbele ya macho yake.
Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno
kiasi kwamba hawezi kugundua
au kuichukia dhambi yake.
Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,
ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.
Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya,
hujitia katika njia ya dhambi
na hakatai lililo baya.
Upendo wako, Ee BWANA,
unafika hadi katika mbingu,
uaminifu wako hadi kwenye anga.
Haki yako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama kilindi kirefu sana.
Ee BWANA, wewe huwahifadhi
mwanadamu na mnyama.
Upendo wako usiokoma
ni wa thamani mno!
Wale wa daraja ya juu na ya chini
miongoni mwa wanadamu
hupata kimbilio katika uvuli wa mbawa zako.
Watajifurahisha katika wingi wa vitu vya nyumbani mwako,
nawe utawanywesha
katika mto wa furaha zako.
Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,
katika nuru yako twaona nuru.
10 Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,
haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.
11 Mguu wa mwenye kiburi na usije dhidi yangu,
wala mkono wa mwovu usinifukuze.
12 Angalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka:
wametupwa chini, hawawezi kuinuka!
Copyright information for Neno