Psalms 37

37:0 Zaburi hii imetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22

Mwisho Wa Mtu Mwovu

(Zaburi Ya Daudi)

1Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu wala usiwaonee wivu watu watendao maovu,
2kwa maana kama majani watanyauka mara,
kama mimea ya kijani watakufa mara.
3Mtumaini BWANA na utende yaliyo mema,
ukae katika nchi ukafurahie malisho salama.
4Jifurahishe katika BWANA naye atakupa
haja za moyo wako.
5Mkabidhi BWANA njia yako,
mtumaini yeye naye atatenda hili:
6yeye atafanya haki yako ing'ae
kama mapambazuko,
hukumu kama jua la adhuhuri.
7Tulia mbele za BWANA
na umngojee kwa uvumilivu;
usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,
wanapotekeleza mipango yao miovu.
8Epuka hasira na uache ghadhabu,
usihangaike, itakuongoza tu kwenye ubaya.
9Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,
bali wale wanaomtumaini BWANA watairithi nchi.
10Bado kitambo kidogo, waovu hawataonekana,
ingawa utawatafuta, hawataonekana.
11Bali wanyenyekevu watairithi nchi
na watafurahia amani tele.
12Waovu hula njama dhidi ya wenye haki
na kuwasagia meno,
13bali Bwana huwacheka waovu,
kwa sababu anajua siku yao inakuja.
14Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde,
ili wawaangushe maskini na wahitaji,
kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu.
15Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe,
na pinde zao zitavunjwa.
16Bora kidogo walichonacho wenye haki
kuliko wingi wa mali
walizo nazo waovu wengi;
17kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa,
lakini BWANA humtegemeza mwenye haki.
18BWANA anazifahamu siku za wanyofu,
na urithi wao utadumu milele.
19Siku za maafa hawatanyauka,
siku za njaa watafurahia kuwa na wingi wa vitu.
20Lakini waovu wataangamia:
Adui za BWANA watatoweka
kama uzuri wa mashamba,
watatoweka,
watatoweka kama moshi.
21Waovu hukopa na hawalipi,
bali wenye haki hutoa kwa ukarimu,
22wale wanaobarikiwa na BWANA watairithi nchi,
bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
23Kama BWANA akipendezwa na njia ya mtu,
huimarisha hatua zake,
24ajapojikwaa, hataanguka,
kwa maana BWANA
humtegemeza kwa mkono wake.
25Nilikuwa kijana na sasa ni mzee,
lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa
au watoto wao wakiomba omba chakula.
26Wakati wote ni wakarimu hukopesha bila masharti,
watoto wao watabarikiwa.
27Acha ubaya na utende wema,
nawe utaishi katika nchi milele.
28Kwa kuwa BWANA huwapenda
wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake.
Watalindwa milele,
lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali;
29wenye haki watairithi nchi,
na kuishi humo milele.
30Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima,
nao ulimi wake huzungumza lililo haki.
31Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake;
nyayo zake hazitelezi.
32Watu waovu huvizia wenye haki,
wakitafuta kuwaua;
33lakini BWANA hatawaacha mikononi mwao
wala hatawaacha wahukumiwe
kuwa wakosa wanaposhtakiwa.
34Umngojee BWANA,
na uishike njia yake.
Naye atakutukuza uirithi nchi,
waovu watakapokatiliwa mbali,
utaliona hilo.
35Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi
kama mwerezi wa Lebanoni,
36lakini alitoweka mara na hakuonekana,
ingawa nilimtafuta,
hakupatikana.
37Watafakari watu wasio na hatia,
wachunguze watu wakamilifu,
kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.
38Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa,
mafanikio yao yatakatiliwa mbali.
39Wokovu wa wenye haki hutoka kwa BWANA,
yeye ni ngome yao wakati wa shida.
40BWANA huwasaidia na kuwaokoa,
huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi,
kwa maana wanamkimbilia.
Copyright information for Neno