Psalms 44

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Wana Wa Kora)

1Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu,
baba zetu wametueleza
yale uliyotenda katika siku zao,
siku za kale.
2Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa katika nchi hii
na ukawapanda baba zetu,
uliangamiza mataifa
na kuwastawisha baba zetu.
3Sio kwa upanga wao waliipata nchi,
wala si mkono wao uliwapatia ushindi;
ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,
na nuru ya uso wako,
kwa kuwa uliwapenda.
4Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,
unayeamuru ushindi kwa Yakobo.
5Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;
kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.
6Siutumaini upinde wangu,
upanga wangu hauniletei ushindi;
7bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,
unawaaibisha watesi wetu.
8Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,
nasi tutalisifu jina lako milele.
9Lakini sasa umetukataa na kutudhili,
wala huendi tena na jeshi letu.
10Umetufanya turudi nyuma mbele ya adui,
nao watesi wetu wametuteka nyara.
11Umetuacha tutafunwe kama kondoo
na umetutawanya katika mataifa.
12Umewauza watu wako kwa fedha kidogo,
wala hukupata faida yo yote kwa mauzo yao.
13Umetufanya lawama kwa jirani zetu,
dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.
14Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa,
mataifa hutikisa vichwa vyao.
15Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa,
na uso wangu umejaa aibu tele,
16kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana,
kwa sababu ya adui,
ambaye anatamani kulipiza kisasi.
17Hayo yote yametutokea,
ingawa tulikuwa hatujakusahau
wala hatujaenda kinyume na Agano lako.
18Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma;
lakini nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.
19Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha
na ukatufunika kwa giza nene.
20Kama tungalikuwa tumelisahau jina la Mungu wetu
au kunyoshea mikono yetu kwa mungu mgeni,
21je, Mungu hangaligundua hili,
kwa kuwa anazijua siri za moyo?
22Hata hivyo kwa ajili yako tunakabiliwa na kifo mchana kutwa;
tunahesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.
23Amka, Ee BWANA! Kwa nini unalala?
Zinduka! Usitukatae milele.
24Kwa nini unauficha uso wako
na kusahau taabu na mateso yetu?
25Tumeshushwa hadi mavumbini,
miili yetu imegandamana na ardhi.
26Inuka na utusaidie,
utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.
Copyright information for Neno