Psalms 46

Mungu Yuko Pamoja Nasi

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Wana Wa Kora. Mtindo Wa Alamothi)

Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa
nayo milima ikiangukia moyoni wa bahari.
Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,
milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.
Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu,
mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.
Mungu yuko katikati yake, hautaanguka,
Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka,
Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka.
BWANA Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Njoni mkaone kazi za BWANA
jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
Anakomesha vita hata miisho ya dunia,
anakata upinde na kuvunjavunja mkuki,
anateketeza ngao kwa moto.
10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;
nitatukuzwa katikati ya mataifa,
nitatukuzwa katika dunia.”
11 BWANA Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi;
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Copyright information for Neno