Psalms 5

Sala Kwa Ajili Ya Ulinzi Wakati Wa Hatari

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Filimbi. Zaburi Ya Daudi)

Ee BWANA, tegea sikio maneno yangu,
uangalie kupiga kite kwangu.
Sikiliza kilio changu ili unisaidie,
Mfalme wangu na Mungu wangu,
kwa maana kwako ninaomba.
Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee BWANA;
asubuhi naleta haja zangu mbele zako,
na kusubiri kwa matumaini.
Wewe si Mungu unayefurahia uovu,
kwako mtu mwovu hataishi.
Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,
unawachukia wote watendao mabaya.
Unawaangamiza wasemao uongo,
wamwagao damu
na wadanganyifu BWANA huwachukia.
Lakini mimi, kwa rehema zako kuu,
nitakuja katika nyumba yako,
kwa unyenyekevu, nitasujudu
kuelekea Hekalu lako takatifu.
Niongoze katika haki yako, Ee BWANA,
kwa sababu ya adui zangu,
nyosha njia yako mbele yangu.
Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika,
mioyo yao imejaa maangamizi.
Koo zao ni kaburi lililo wazi,
kwa ndimi zao hunena udanganyifu.
10 Uwatangaze kwamba wana hatia, Ee Mungu!
Hila zao ziwe anguko lao wenyewe.
Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi,
kwa kuwa wamekuasi wewe.
11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,
waimbe kwa shangwe daima.
Ueneze ulinzi wako juu yao,
ili wale wapendao jina lako
wapate kukushangilia.
12 Kwa hakika, Ee BWANA, unawabariki wenye haki,
unawazunguka kwa wema wako kama ngao.
Copyright information for Neno