Psalms 50

Ibada Ya Kweli

(Zaburi Ya Asafu)

Mwenye Nguvu, Mungu, BWANA,
asema na kuiita dunia,
tangu maawio ya jua
hadi mahali pake liendapo kutua.
Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,
Mungu anaangaza.
Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,
moto uteketezao unamtangulia,
akiwa amezungukwa na tufani kali.
Anaziita mbingu zilizo juu
na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:
“Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,
waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
Nazo mbingu zinatangaza haki yake,
kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.
“Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,
Ee Israeli, nami nitawashuhudia dhidi yenu:
Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.
Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,
au sadaka zako za kuteketezwa,
ambazo daima ziko mbele zangu.
Sina haja ya fahali wa banda lako,
au mbuzi wa zizi lako.
10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,
nayo makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.
11 Ninamjua kila ndege mlimani,
nao viumbe wa kondeni ni wangu.
12 Kama ningekuwa na njaa nisingewaambia ninyi,
kwa maana ulimwengu ni wangu,
pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.
13 Je, mimi hula nyama ya mafahali
au kunywa damu ya mbuzi?
14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,
timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,
15 na uniite siku ya taabu;
nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”
16 

Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema: “Una haki gani kunena sheria zangu
au kuchukua Agano langu midomoni mwako?
17 Unachukia mafundisho yangu
na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
18 Unapomwona mwizi, unaungana naye,
unapiga kura yako pamoja na wazinzi.
19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya
na kuuongoza ulimi wako kwa hila.
20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako
na kumsingizia mwana wa mama yako.
21 Mambo haya unayafanya nami nimekaa kimya,
ukafikiri Mimi nami ni kama wewe.
Lakini nitakukemea
na kuweka mashtaka mbele yako.
22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,
ama sivyo nitawararua vipande vipande,
wala hapatakuwepo na ye yote wa kuwaokoa:
23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,
naye aiandaa njia yake jinsi ipasavyo
nitamwonyesha wokovu wa Mungu.”


Copyright information for Neno