Psalms 52

Hukumu Ya Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Daudi Baada Ya Doegi, Mwedomu, Kumwendea Sauli Na Kumjulisha Kuwa Daudi Amekwenda Nyumbani Kwa Abimeleki)

1Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?
Kwa nini unajivuna mchana kutwa,
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
2Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi,
ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.
3Unapenda mabaya kuliko mema,
uongo kuliko kusema kweli.
4Unapenda kila neno lenye kudhuru,
ewe ulimi wenye hila!
5Hakika Mungu atakushusha chini
kwa maangamizi ya milele:
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu
kutoka katika hema yako,
atakung'oa kutoka nchi ya walio hai.
6Wenye haki wataona na kuogopa,
watamcheka, wakisema,
7“Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,
bali alitumainia wingi wa utajiri wake
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

Neema Ya Mungu

8Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni
unaostawi katika nyumba ya Mungu,
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma
milele na milele.
9Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.
Copyright information for Neno