Psalms 55

Maombi Ya Mtu Aliyesalitiwa Na Rafiki

(Kwa Mwimbishaji: Na Ala Za Uimbaji. Utenzi Wa Daudi)

Ee Mungu, sikiliza maombi yangu,
wala usidharau hoja yangu,
nisikie na unijibu.
Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa
kwa sauti ya adui,
kwa kukaziwa macho na waovu,
kwa sababu wananiletea mateso juu yangu
na kunitukana kwa hasira zao.
Moyo wangu umejaa uchungu,
hofu ya kifo imenishambulia.
Woga na kutetemeka vimenizunguka,
hofu kuu imenigharikisha.
Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa!
Ningeruka niende mbali kupumzika.
Ningalitorokea mbali sana
na kukaa jangwani,
ningaliharakisha kwenda mahali pa salama,
mbali na tufani kali na dhoruba.”
Ee BWANA, uwatahayarishe waovu
na uwafanye maadui wasielewane semi zao,
maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.
10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake,
uovu na dhuluma vimo ndani yake.
11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini,
vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.
12 Kama aliyenitukana ni adui yangu ningevumilia,
kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,
ningejificha asinione.
13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,
mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
14 ambaye wakati fulani tulifurahia ushirika mzuri
tulipokuwa tukienda katikati ya umati
hekaluni mwa Mungu.
15 Kifo na kiwajilie adui zangu ghafula,
na washuke kuzimu wangali hai,
kwa maana ubaya upo ndani yao.
16 Lakini ninamwita Mungu,
naye BWANA huniokoa.
17 Jioni, asubuhi na adhuhuri
ninalia kwa huzuni,
naye husikia sauti yangu.
18 Huniokoa nikawa salama kutoka katika vita
vilivyopangwa dhidi yangu,
ingawa watu wengi hunipinga.
19 Mungu anayemiliki milele,
atawasikia na kuwaadhibu,
watu ambao hawabadilishi njia zao
na wala hawana hofu ya Mungu.
20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake,
naye huvunja agano lake.
21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi,
hata hivyo vita vimo moyoni mwake,
maneno yake mororo kuliko mafuta,
hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.
22 Mtwike BWANA fadhaa zako,
naye atakutegemeza,
hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.
23 Lakini wewe, Ee Mungu,
utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.
Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,
hawataishi nusu ya siku zao.
Lakini mimi, ninakutumaini wewe.
Copyright information for Neno