Psalms 57

Kuomba Msaada

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu! Utenzi Wa Daudi Baada Ya Kumponyoka Sauli Pangoni)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.
Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia
mpaka maafa yapite.
Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,
Mungu atimizaye makusudi yake kwangu.
Hutuma kutoka mbinguni na kuniokoa,
akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;
Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
Niko katikati ya simba,
nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu,
watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,
ambao ndimi zao ni panga kali.
Ee Mungu, utukuzwe, juu mbinguni,
utukufu wako na uenee duniani kote.
Waliitegea miguu yangu nyavu,
nikainamishwa chini na dhiki.
Wamechimba shimo katika njia yangu,
lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
Ee Mungu, moyo wangu uko imara,
naam moyo wangu uko imara,
nitaimba na kupiga vinanda.
Amka, nafsi yangu!
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
Nitakusifu wewe, Ee BWANA,
katikati ya mataifa,
nitaimba habari zako,
katikati ya jamaa za watu.
10 Kwa maana upendo wako,
waenea hadi mbinguni,
uaminifu wako unazifikia anga.
11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,
utukufu wako na uwe duniani pote.
Copyright information for Neno