Psalms 58

Mungu Kuwaadhibu Waovu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu! Utenzi Wa Daudi)

Enyi watawala, Je, kweli mwanena kwa haki?
Je, mnahukumu kwa unyofu
miongoni mwa watu?
La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu,
na mikono yenu hupima jeuri duniani.
Waovu ni wapotovu hata tangu kuzaliwa kwao,
toka tumboni mwa mama zao
ni wakaidi na husema uongo.
Sumu yao ni kama sumu ya nyoka,
kama ile ya nyoka mwenye sumu kali
ambaye ameziba masikio yake,
ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi,
hata kama mganga angeagua
kwa ustadi kiasi gani.
Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao;
Ee BWANA, vunja meno makali ya hao simba!
Wana na watoweke kama maji yatiririkayo kwa kasi,
wavutapo pinde zao,
mishale yao na iwe butu.
Kama konokono ayeyukavyo akitembea,
kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu,
na wasilione jua.
Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba,
zikiwa mbichi au kavu,
waovu watakuwa
wamefagiliwa mbali.
10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi,
wakati wakichovya nyayo zao
katika damu ya waovu.
11 Ndipo wanadamu watasema,
“Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu,
hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”
Copyright information for Neno