Psalms 60

Kuomba Kuokolewa

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Shushani Eduthi. Utenzi Wa Daudi Wa Kufundisha Wakati Alipopigana Na Waaramu Kutoka Aramu-Naharaimu Na Aramu-Soba, Yoabu Aliporudi Nyuma Na Kuwaua Waedomu 12,000 Katika Bonde La Chumvi)

Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,
umekasirika, sasa uturejeshe upya!
Umetetemesha nchi na kuipasua;
uiponye na kutengeneza mavunjiko yake,
kwa maana inatetemeka.
Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa;
umetunywesha mvinyo unaotufanya tupepesuke.
Kwa wale wanaokucha wewe,
umewainulia bendera,
ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.
Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao waweze kuokolewa.
Mungu amenena kutoka mahali patakatifu pake:
“Kwa furaha kuu nitaigawa Shekemu
na kupima Bonde la Sukothi.
Gileadi ni yangu na Manase ni yangu,
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
na Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
Moabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nami nitashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wenye maboma?
Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?
10 Ee Mungu, si wewe, wewe uliyetukataa sisi
na hutoki tena na majeshi yetu?
11 Tupe msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai.
12 Mungu akiwa pamoja nasi tutajipatia ushindi,
naye atawakanyaga chini adui zetu.
Copyright information for Neno