Psalms 66

Kusifu Mungu Kwa Ajili Ya Wema Wake

(Kwa Mwimbishaji: Wimbo. Zaburi)

1Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
2Imbeni utukufu wa jina lake;
mpeni sifa zake kwa utukufu!
3Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!
Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba
adui wananyenyekea mbele zako.
4Dunia yote yakusujudia,
wanakuimbia wewe sifa,
wanaliimbia sifa jina lako.”
5Njoni mwone yale Mungu aliyoyatenda,
mambo ya kutisha aliyoyatenda
miongoni mwa wanadamu!
6Alifanya bahari kuwa nchi kavu,
wakapita kati ya maji kwa miguu,
njoni, tumshangilie.
7Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,
macho yake huangalia mataifa yote,
waasi na wasithubutu kujiinua dhidi yake.
8Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,
sauti ya sifa yake na isikike,
9ameyahifadhi maisha yetu
na kuizuia miguu yetu kuteleza.
10Ee Mungu, wewe ulitujaribu,
ukatusafisha kama fedha.
11Umetuingiza kwenye nyavu
na umetubebesha mizigo mizito
migongoni mwetu.
12Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,
tulipita kwenye moto na kwenye maji,
lakini ulituleta kwenye nchi
iliyojaa utajiri tele.
13Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa
na kukutimizia nadhiri zangu:
14nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi
na nilizotamka kwa kinywa changu
nilipokuwa katika shida.
15Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono
na sadaka za kondoo waume,
nitakutolea mafahali na mbuzi.
16Njoni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,
nami niwaambie aliyonitendea.
17Nilimlilia kwa kinywa changu,
sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
18Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,
Bwana asingekuwa amenisikiliza;
19lakini hakika Mungu amenisikiliza
na amesikia sauti yangu katika maombi.
20Sifa apewe Mungu,
ambaye hakulikataa ombi langu
wala kunizuilia upendo wake!
Copyright information for Neno