Psalms 68

Wimbo Wa Taifa Wa Shangwe Kwa Ushindi

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi ya Daudi. Wimbo)

1Mungu na ainuke, watesi wake na watawanyike,
adui zake na wakimbie mbele zake.
2Kama vile moshi upeperushwavyo na upepo,
vivyo hivyo uwapeperushe mbali,
kama vile nta iyeyukavyo kwenye moto,
vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.
3Bali wenye haki na wafurahi,
washangilie mbele za Mungu,
na wafurahi na kushangilia.
4Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake,
mwinueni juu yeye aendeshwaye juu ya mawingu,
jina lake ni BWANA,
furahini mbele zake.
5Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,
ni Mungu katika makao yake matakatifu.
6Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,
huwaongoza wafungwa wakiimba,
bali waasi huishi katika nchi kame.
7Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako,
ulipopita nyikani,
8dunia ilitikisika,
mbingu zikanyesha mvua,
mbele za Mungu, Mungu wa Mlima Sinai,
mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.
9Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi
na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.
10Ee Mungu, watu wako waliishi huko,
kwa wingi wa utajiri wako
uliwapa maskini mahitaji yao.
11Bwana alitangaza neno,
waliolitangaza neno hilo walikuwa kundi kubwa:
12“Wafalme na majeshi walikimbia upesi,
watu waliobaki kambini waligawana nyara.
13Hata ulalapo katikati ya mioto ya kambini,
mabawa ya njiwa wangu, yamefunikwa kwa fedha,
manyoya yake kwa dhahabu ing'aayo.”
14Wakati Mwenyezi
68:14 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania
alipowatawanya wafalme katika nchi,
ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Salmoni.
15Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka,
milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.
16Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka,
kwa nini mnakazia macho kwa wivu,
katika mlima Mungu anaochagua kutawala,
ambako BWANA mwenyewe ataishi milele?
17Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu,
na maelfu ya maelfu;
Bwana amekuja kutoka Sinai
kuja katika patakatifu pake.
18Ulipopanda juu, uliteka mateka,
ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu,
hata kutoka kwa wale walioasi,
ili wewe, Ee BWANA, upate kuishi huko.
19Sifa apewe Bwana, Mungu Mwokozi wetu,
ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.
20Mungu wetu ni Mungu aokoaye,
BWANA Mwenyezi hutuokoa na kifo.
21Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake,
vichwa vya hao waendao katika njia za dhambi.
22Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani;
nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,
23ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako,
huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”
24Ee Mungu, maandamano yako yameonekana,
maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu,
yakielekea katika mahali patakatifu pake.
25Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda,
pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.
26Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa,
msifuni BWANA katika kusanyiko la Israeli.
27Kuna kabila dogo la Benyamini, likiwaongoza,
wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda,
hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.
28Ee Mungu, amuru uwezo wako,
Ee Mungu tuonyeshe nguvu zako,
kama ulivyofanya hapo awali.
29Kwa sababu ya Hekalu lako la Yerusalemu
wafalme watakuletea zawadi.
30Mkemee mnyama aliyeko kwenye manyasi,
kundi la mafahali katikati ya ndama za mataifa.
Wakiwa wamenyenyekea na walete minara ya madini ya fedha.
Tawanya mataifa yapendayo vita.
31Wajumbe watakuja kutoka Misri,
Kushi
68.31 Kushi hapa ina maana maeneo ya Nile ya juu, yaani Ethiopia
atajisalimisha kwa Mungu.
32Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia,
mwimbieni Bwana sifa,
33mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu,
yeye angurumaye kwa sauti kuu.
34Tangazeni uwezo wa Mungu,
ambaye fahari yake iko juu ya Israeli,
ambaye uwezo wake uko katika anga.
35Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,
Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.
Mungu Asifiwe!
Copyright information for Neno