Psalms 69

Kilio Cha Kuomba Msaada Wakati Wa Dhiki

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi)

Ee Mungu, uniokoe, kwa maana maji
yamenifika shingoni.
Ninazama kwenye vilindi vya matope,
pasipo mahali pa kukanyaga;
nimefika kwenye maji makuu,
mafuriko yamenigharikisha.
Nimechoka kwa kuomba msaada,
koo langu limekauka.
Macho yangu yanafifia,
nikimtafuta Mungu wangu.
Wale wanaonichukia bila sababu
ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;
wengi ni adui bila sababu,
wale wanaotafuta kuniangamiza.
Ninalazimishwa kurudisha
kitu ambacho sikuiba.
Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,
wala maovu yangu hayakufichika kwako.
Ee Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
wakutumainio wasiaibishwe
kwa ajili yangu;
wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu,
Ee Mungu wa Israeli.
Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,
aibu imefunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe,
kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,
matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.
10 Ninapolia na kufunga,
wao hunitukana kwa kufanya hivyo.
11 Nilipovaa nguo ya gunia,
nilikuwa kitu cha kudharauliwa na watu.
12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,
nimekuwa wimbo wa walevi.
13 Lakini Ee BWANA, ninakuomba,
kwa wakati ukupendezao,
katika upendo wako mkuu;
Ee Mungu, unijibu
kwa wokovu wako wa hakika.
14 Uniokoe katika matope,
usiniache nizame;
niokoe na hao wanichukiao,
kutoka kwenye vilindi vya maji.
15 Usiache mafuriko yanigharikishe
au vilindi vinimeze,
au shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.
16 Ee BWANA, unijibu, kwa wema wa upendo wako;
kwa huruma zako nyingi unigeukie.
17 Usimfiche mtumishi wako uso wako,
uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.
18 Njoo karibu na uniokoe,
nikomboe kwa sababu ya adui zangu.
19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa,
kufedheheshwa na kuaibishwa,
adui zangu wote unawajua.
20 Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa,
nimetafuta wa kunihurumia,
lakini sikumpata ye yote,
wa kunituliza, lakini sikumpata ye yote.
21 Waliweka nyongo katika chakula changu
na walinipa siki nilipokuwa na kiu.
22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,
nayo iwe upatilizo na tanzi.
23 Macho yao yatiwe giza ili wasione,
migongo yao na ipinde milele.
24 Uwamwagie ghadhabu yako,
hasira yako kali na iwapate.
25 Mahali pao na pawe mahame,
asiwepo ye yote atakayeishi katika mahema yao.
26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,
na kuzungumza juu ya maumivu
ya wale uliowaumiza.
27 Walipize uovu juu ya uovu,
usiwaache washiriki katika wokovu wako.
28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima
na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.
29 Mimi niko katika maumivu na dhiki;
Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.
30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.
31 Hili litampendeza BWANA kuliko ng'ombe dume,
zaidi ya fahali akiwa
na pembe na kwato zake.
32 Maskini wataona na kufurahi,
ninyi mnaomtafuta Mungu,
mioyo yenu na iishi!
33 BWANA huwasikia wahitaji
na wala hadharau watu wake waliotekwa.
34 Mbingu na dunia na vimsifu,
bahari na vyote viendavyo ndani yake,
35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni
na kuijenga tena miji ya Yuda.
Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki.
36 Watoto wa watumishi wake watairithi
na wale wote walipendao jina lake
wataishi humo.
Copyright information for Neno