Psalms 71

Kuomba Ulinzi Na Msaada Siku Zote Za Maisha

Ee BWANA, nimekukimbilia wewe,
usiniache nikaaibika kamwe.
Kwa haki yako uniponye na kuniokoa,
unitegee sikio lako uniokoe.
Uwe mwamba wa kimbilio langu,
mahali nitakapokimbilia kila wakati;
toa amri ya kuniokoa, kwa kuwa wewe
ni mwamba wangu
na ngome yangu.
Ee Mungu wangu uniokoe kutoka kwenye mkono wa mwovu,
kutoka kwenye makucha
ya watu wabaya na wakatili.
Ee BWANA Mwenyezi, kwa kuwa umekuwa tumaini langu,
tegemeo langu tangu ujana wangu.
Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe,
ulinitoa tumboni mwa mama yangu.
Nitakusifu wewe daima.
Nimekuwa kama kioja kwa wengi,
lakini wewe ni kimbilio langu imara.
Kinywa changu kimejazwa sifa zako,
nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.
Usinitupe wakati wa uzee,
wala usiniache nguvu zangu zinapopungua.
10 Kwa maana adui zangu wananisengenya,
wale wanaonivizia kuniua wafanya hila.
11 Wanasema, “Mungu amemwacha,
mkimbilieni mumkamate,
kwani hakuna wa kumwokoa.”
12 Ee Mungu, usiwe mbali nami,
Ee Mungu wangu njoo haraka kunisaidia.
13 Washtaki wangu na waangamie kwa aibu,
wale wanaotaka kunidhuru
na wafunikwe kwa dharau na fedheha.
14 Lakini mimi, nitatumaini siku zote,
nitakusifu zaidi na zaidi.
15 Kinywa changu kitasimulia haki yako,
wokovu wako mchana kutwa,
ingawa sifahamu kipimo chake.
16 Ee BWANA Mwenyezi, nitakuja
na kutangaza matendo yako makuu,
nitatangaza haki yako, yako peke yako.
17 Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu,
hadi leo ninatangaza matendo yako ya ajabu.
18 Ee Mungu, usiniache,
hata niwapo mzee wa mvi,
mpaka nitangaze uwezo wako kwa kizazi kijacho,
nguvu zako kwa wote watakaokuja baadaye.
19 Ee Mungu, haki yako imefika juu katika mbingu,
wewe ambaye umefanya mambo makuu.
Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
20 Ingawa umenifanya nipate taabu, nyingi na chungu,
utanihuisha tena,
kutoka vilindi vya dunia
utaniinua tena.
21 Utaongeza heshima yangu
na kunifariji tena.
22 Ee Mungu wangu, nitakusifu kwa kinubi
kwa ajili ya uaminifu wako;
Ee Mtakatifu Pekee wa Israeli,
nitakuimbia sifa kwa zeze.
23 Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha
ninapokuimbia sifa,
mimi, ambaye umenikomboa.
24 Ulimi wangu utasimulia matendo yako ya haki
mchana kutwa,
kwa maana wale waliotaka kunidhuru,
wameaibishwa na kufadhaishwa.
Copyright information for Neno