Psalms 74

Maombi Kwa Ajili Ya Taifa Kuokolewa

(Utenzi Wa Asafu)

1Ee Mungu, mbona umetukataa milele?
Mbona hasira yako inawaka na kutoka moshi
juu ya kondoo wa malisho yako?
2Kumbuka watu uliowanunua zamani,
kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa:
Mlima Sayuni, ambamo uliishi.
3Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu,
uharibifu wote huu ambao adui ameuleta
katika mahali patakatifu.
4Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi,
wanaweka bendera zao kama alama.
5Walifanya kama watu wanaotumia mashoka
kukata kichaka chote cha miti.
6Walivunjavunja milango yote iliyonakishiwa
kwa mashoka na vishoka vyao.
7Waliteketeza kabisa mahali patakatifu,
wakayanajisi makao ya Jina lako.
8Walisema mioyoni mwao,
“Tutawaponda kabisa!”
Walichoma kila mahali ambapo Mungu
aliabudiwa katika nchi.
9Hatukupewa ishara za miujiza;
hakuna manabii waliobaki,
hakuna ye yote kati yetu ajuaye
kwamba hali hii itachukua muda gani.
10Ee Mungu, mtesi atakudhihaki mpaka lini?
Je, adui watalitukana jina lako milele?
11Kwa nini unazuia mkono wako,
mkono wako wa kuume?
Uutoe kutoka katika makunjo ya vazi lako
na uwaangamize!
12Lakini wewe, Ee Mungu,
ni mfalme wangu tangu zamani,
unaleta wokovu duniani.
13Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako;
ulivunja vichwa vya wanyama wakubwa wa kutisha katika maji.
14Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani
74.14 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa

nawe ukamtoa kama chakula
cha viumbe vya jangwani.
15Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito,
ulikausha mito ambayo ilikuwa ikitiririka daima.
16Mchana ni wako, nao usiku ni wako pia,
uliweka jua na mwezi.
17Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia,
ulifanya kiangazi na masika.
18Ee BWANA, kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki,
jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako.
19Usiukabidhi uhai wa njiwa wako
kwa wanyama wakali wa mwitu;
usisahau kabisa uhai wa watu wako
wanaoteseka milele.
20Likumbuke agano lako,
maana mara kwa mara mambo ya jeuri
yamejaa katika sehemu za giza katika nchi.
21Usiruhusu walioonewa warudi nyuma kwa aibu;
maskini na wahitaji na walisifu jina lako.
22Inuka, Ee Mungu, ujitetee;
kumbuka jinsi wapumbavu
wanavyokudhihaki mchana kutwa.
23Usipuuze makelele ya watesi wako,
ghasia za adui zako,
zinazoinuka mfululizo.
Copyright information for Neno