Psalms 76

Mungu Wa Israeli Ni Mhukumu Wa Dunia Yote

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Nyuzi Za Muziki. Zaburi Ya Asafu. Wimbo)

Katika Yuda Mungu anajulikana,
jina lake ni kuu katika Israeli.
Hema lake liko Salemu,
makao yake katika Sayuni.
Huko alivunja mishale imetametayo,
ngao na panga, silaha za vita.
Wewe unang'aa kwa mwanga,
mwenye fahari zaidi ya milima
yenye utajiri wa wanyama pori.
Mashujaa hulala wametekwa nyara,
hulala usingizi wao wa mwisho;
hakuna hata mmoja wa watu wa vita
anayeweza kuinua mikono yake.
Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo,
farasi na gari la vita vilikaa kimya.
Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa.
Ni nani awezaye kusimama mbele yako
wakati umekasirika?
Kutoka mbinguni ulitamka hukumu,
nayo nchi ikaogopa ikawa kimya,
wakati wewe, Ee Mungu,
ulipoinuka kuhukumu,
kuwaokoa wote walioonewa katika nchi.
10 Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu
inakuletea sifa,
na masalia ya ghadhabu yako
utajifunga mshipi.
11 Wekeni nadhiri kwa BWANA Mungu wenu na kuzitimiza;
nchi zote za jirani na walete zawadi
kwa yeye astahiliye kuogopwa.
12 Huvunja roho za watawala;
anaogopwa na wafalme wa dunia.
Copyright information for Neno