Psalms 81

Wimbo Wa Sikukuu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Gitithi. Zaburi Ya Asafu)

Mwimbieni kwa furaha Mungu aliye nguvu yetu;
mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo!
Anzeni wimbo, pigeni matari,
pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri.
Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume
wakati wa Mwandamo wa Mwezi,
na wakati wa mwezi mpevu,
katika siku ya Sikukuu yetu;
hii ni amri kwa Israeli,
agizo la Mungu wa Yakobo.
Aliiweka iwe kama sheria kwa Yosefu
alipotoka dhidi ya Misri,
huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa.
Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao;
mikono yao iliwekwa huru kutoka kwenye kikapu.
Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa,
nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo;
nilikujaribu katika maji ya Meriba.
“Enyi watu wangu sikieni, nami nitawaonya:
laiti kama mngenisikiliza, Ee Israeli!
Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu;
msimsujudie mungu wa kigeni.
10 Mimi ni BWANA Mungu wako,
niliyekutoa katika nchi ya Misri.
Panua sana kinywa chako
nami nitakijaza.
11 “Lakini watu wangu hawakutaka kunisikiliza;
Israeli hakutaka kunitii.
12 Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao
wafuate mashauri yao wenyewe.
13 “Laiti kama watu wangu wangalinisikiliza,
kama Israeli wangalifuata njia zangu,
14 ningaliwatiisha adui zao kwa haraka
na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao!
15 Wale wanaomchukia BWANA wangalinywea mbele zake,
na adhabu yao ingedumu milele.
16 Bali ninyi mngalilishwa ngano iliyo bora,
na kuwatosheleza kwa asali itokayo kwenye mwamba.”
Copyright information for Neno