Psalms 88

Kilio Kwa Ajili Ya Kuomba Msaada

Ee BWANA, Mungu uniokoaye,
nimelia mbele zako usiku na mchana.
Maombi yangu na yafike mbele zako,
utegee kilio changu sikio lako.
Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,
na maisha yangu yanakaribia kaburi
88.3 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
.
Nimehesabiwa miongoni mwa wale waendao shimoni,
niko kama mtu asiye na nguvu.
Nimetengwa pamoja na wafu,
kama waliochinjwa walalao kaburini,
ambao huwakumbuki tena,
ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.
Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,
katika vina vya giza nene.
Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,
umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.
Umenitenga na rafiki zangu wa karibu kuliko wote
na kunifanya wanisukumie mbali.
Nimezuiliwa wala siwezi kutoroka;
nuru ya macho yangu
imefifia kwa ajili ya huzuni.
Ee BWANA, ninakuita kila siku,
ninakunyoshea wewe mikono yangu.
10 Je, huwaonyesha wafu maajabu yako?
Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?
11 Je, upendo wako hutangazwa kaburini,
uaminifu wako katika uharibifu?
12 Je, maajabu yako hujulikana mahali pa gizani,
au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?
13 Lakini ninakulilia wewe, Ee BWANA unisaidie,
asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
14 Ee BWANA, kwa nini unanikataa
na kunificha uso wako?
15 Tangu ujana wangu nimeteseka nikakaribia kifo;
nimepatwa na hofu zako nami nimekata tamaa.
16 Ghadhabu yako imepita juu yangu;
hofu zako zimeniangamiza.
17 Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;
zimenimeza kabisa.
18 Umeniondolea marafiki na wapendwa wangu;
giza limekuwa ndilo rafiki yangu wa karibu kuliko wote.
Copyright information for Neno