Psalms 93

Mungu Mfalme

BWANA anatawala, amejivika utukufu;
BWANA amejivika utukufu
tena amejivika nguvu.
Dunia imewekwa imara,
haitaondoshwa.
Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani;
wewe umekuwako tangu milele.
Bahari zimeinua, Ee BWANA,
bahari zimeinua sauti zake;
bahari zimeinua sauti za mawimbi yake.
Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu,
ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari:
BWANA aishiye juu sana ni mkuu.
Ee BWANA, sheria zako ni imara;
utakatifu umepamba nyumba yako
pasipo mwisho.
Copyright information for Neno