Psalms 94

Mungu Mlipiza Kisasi Kwa Ajili Ya Wenye Haki

Ee BWANA, ulipizaye kisasi,
Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
Ee mhukumu wa dunia, inuka,
uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
Hata lini, waovu, Ee BWANA,
hata lini waovu watashangilia?
Wanamimina maneno ya kiburi,
watenda mabaya wote wamejaa majivuno.
Ee BWANA, wanawaponda watu wako,
wanawaonea urithi wako.
Wanamchinja mjane na mgeni,
na kuwaua yatima.
Nao husema, “BWANA haoni,
Mungu wa Yakobo hafahamu.”
Sikia, enyi wajinga miongoni mwa watu,
enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
Je, aliyeweka sikio asisikie?
Aliyeumba jicho asione?
10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?
Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11 BWANA anajua mawazo ya mwanadamu,
anajua ya kwamba hayafai.
12 Ee BWANA, heri mtu anayeadhibishwa na wewe,
mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
13 unampa utulivu siku za shida,
mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa
kwa ajili ya mwovu.
14 Kwa kuwa BWANA hatawakataa watu wake,
hatauacha urithi wake.
15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,
wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?
Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
17 Kama BWANA asingelinisaidia upesi,
ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.
18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”
Ee BWANA, upendo wako ulinishikilia.
19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,
faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,
ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
21 Huungana kuwashambulia wenye haki,
kuwahukumu kufa wasio na hatia.
22 Lakini BWANA amekuwa ngome yangu,
na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao
na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;
BWANA Mungu wetu atawaangamiza.
Copyright information for Neno