Psalms 96

Mungu Mfalme Mkuu

1Mwimbieni BWANA wimbo mpya;
mwimbieni BWANA dunia yote.
2Mwimbieni BWANA, lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu
miongoni mwa mataifa yote.
4Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini BWANA aliziumba mbingu.
6Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
7Mpeni BWANA, enyi jamaa za mataifa,
mpeni BWANA utukufu na nguvu.
8Mpeni BWANA utukufu unaostahili jina lake;
leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9Mwabuduni BWANA katika uzuri wa utakatifu wake;
dunia yote na itetemeke mbele zake.
10Katikati ya mataifa semeni, “BWANA anatawala.”
Ulimwengu ameuweka imara
hauwezi kusogezwa,
atawahukumu mataifa kwa uadilifu.
11Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
bahari na ivume,
na vyote vilivyomo ndani yake;
12mashamba na yashangilie,
pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha,
13vitaimba mbele za BWANA
kwa maana anakuja,
anakuja kuhukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki
na mataifa katika kweli yake.
Copyright information for Neno