Psalms 99

Mungu Mfalme Mkuu

BWANA anatawala,
mataifa na yatetemeke;
anaketi kwenye kiti cha enzi katikati ya makerubi,
dunia na itikisike.
BWANA ni mkuu katika Sayuni;
ametukuzwa juu ya mataifa yote.
Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa:
yeye ni mtakatifu!
Mfalme mwenye nguvu hupenda haki,
wewe umethibitisha adili;
katika Yakobo umefanya
yaliyo haki na sawa.
Mtukuzeni BWANA Mungu wetu,
na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;
yeye ni mtakatifu.
Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake,
Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake;
walimwita naye aliwajibu.
Alizungumza nao kutoka katika nguzo ya wingu;
walizishika sheria zake na amri alizowapa.
Ee BWANA, wetu,
ndiwe uliyewajibu,
kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,
ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.
Mtukuzeni BWANA Mungu wetu
na mwabudu kwenye mlima wake mtakatifu,
kwa maana BWANA Mungu wetu ni mtakatifu.
Copyright information for Neno