Revelation of John 12

Mwanamke Na Joka

1Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. 2Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5Yule mwanamke akazaa mtoto mwanamume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. 6Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

Malaika Mikaeli Amshinda Yule Joka

7Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni. 9Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwenguni wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

Ushindi Mbinguni Watangazwa

10Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: “Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja
na mamlaka ya Kristo wake.
Kwa kuwa ametupwa chini
mshtaki wa ndugu zetu,
anayewashtaki mbele za Mungu
usiku na mchana.
11Nao wakamshinda
kwa damu ya Mwana-Kondoo
na kwa neno la ushuhuda wao.
Wala wao hawakuyapenda maisha yao
hata kufa.
12Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu
na wote wakaao humo!
Lakini ole wenu nchi na bahari,
kwa maana huyo Shetani ameshuka kwenu,
akiwa amejaa ghadhabu,
kwa sababu anajua ya kuwa
muda wake ni mfupi!”13Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanamume. 14Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko nyikani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu
12.14 Maana yake ni miaka mitatu na nusu
, wakati ambako yule joka hawezi kufika.
15Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko. 16Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake. 17Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke, likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.

Copyright information for Neno