Revelation of John 2

Kwa Kanisa Lililoko Efeso

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:

“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea katikati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.
Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. Nami najua umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.

“Lakini nina neno juu yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. Kumbuka basi ni wapi ulikoanguka! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami nayachukia.

“Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye atakayeshinda, nitampa haki ya kula matunda ya mti wa uzima, ambao uko katika paradiso
2.7Paradiso hapa ina maana ya Bustani, yaani shamba dogo la miti izaayo matunda
ya Mungu.

Kwa Kanisa Lililoko Smirna

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.
Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, wao ni sinagogi la Shetani. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia Shetani atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu, hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

11 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa na mauti ya pili.

Kwa Kanisa Lililoko Pergamo

12 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga wenye makali kuwili.
13 Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji wenu, ambako ndiko anakokaa Shetani.

14 “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati. 15 Vivyo hivyo unao wale wayashikao mafundisho ya Wanikolai. 16 Basi tubuni! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.

17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa yeye jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.

Kwa Kanisa Lililoko Thiatira

18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika:

“Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana.
19 Nayajua matendo yako, upendo wako, imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.

20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili atubie uasherati wake, lakini hataki. 22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, nami nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. 23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia za watu na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. 24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo wengine wanayoyaita mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wo wote juu yenu): 25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja.

26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa: 27 “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma,
atawavunja vipande vipande
kama chombo cha udongo’:


kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu.
28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi. 29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

Copyright information for Neno