Revelation of John 3

Kwa Kanisa Lililoko Sardi

“Kwa malaika wa Kanisa lililoko Sardi andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na zile Roho saba
3.1 Roho saba za Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake
za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.
Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwivi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.

“Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao, nami sitafuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake. Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Filadelfia

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.
Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu. Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, waje wapige magoti miguuni pako, nao watatambua ya kwamba nimekupenda. 10 Kwa kuwa umelishika neno la saburi yangu nitakulinda hata utoke katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote ili kuwajaribu wote wakaao duniani.

11 “Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako. 12 Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya. 13 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Laodikia

14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa baridi au moto. 16 Hivyo kwa kuwa u uvuguvugu, kwamba wewe si baridi wala si moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu cho chote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Kwa hiyo nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri na mavazi meupe ili uyavae, upate kuficha aibu ya uchi wako na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu ye yote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.

21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.”

Copyright information for Neno