Revelation of John 8

Lakiri Ya Saba Na Chetezo Cha Dhahabu

Mwana-Kondoo alipoivunja ile lakiri ya saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.

Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.

Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya Watakatifu wote, juu ya ile madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele ya kile kiti cha enzi. Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika. Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwenye ile madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la nchi.

TARUMBETA SABA

Tarumbeta Ya Kwanza

Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.

Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea na majani yote mabichi yakateketea.

Tarumbeta Ya Pili

Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.

Tarumbeta Ya Tatu

10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. 11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

Tarumbeta Ya Nne

12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota, zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.

13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”

Copyright information for Neno