Romans 10

1Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe. 2Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wanajuhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. 3Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

Wokovu Ni Kwa Ajili Ya Wote

5Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye mambo hayo ataishi kwa hayo.” 6Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7“au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8Lakini andiko lasemaje? “Lile neno li karibu nawe, li kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, ni lile neno la imani tunalolihubiri. 9Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11Kama yasemavyo Maandiko, “Ye yote amwaminiye hatatahayarika.” 12Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokoka.”

14Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyaoandikwa, “Ni mizuri mno miguu ya hao wanaohubiri Injili ya amani na kuleta habari ya mema!”

16Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17Basi, imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. 18Lakini nauliza, Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani kote,
nayo maneno yao yamefika
hadi miisho ya ulimwengu.”


19Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale
ambao si taifa.
Nitawakasirisha kwa taifa la watu
wasio na ufahamu.”20Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Watu wale waliokuwa hawanitafuti, wamenipata;
nimejidhihirisha kwa watu
wale waliokuwa hawaniulizii.”21Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyoshea
watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”


Copyright information for Neno