Ruth 1

Naomi Na Ruthu

1Wakati Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi, akaondoka mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu. 2Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu wakaishi huko.

3Elimeleki mumewe Naomi akafa, Naomi akabaki na wanawe wawili. 4Nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya miaka kumi, 5Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.

6Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba BWANA amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakweze wakajiandaa kurudi nyumbani. 7Yeye na wakweze wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.

8Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe zake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani kwa mama yake. BWANA na awatendee fadhili kama mlivyowatendea hao waliofariki pamoja na mimi. 9BWANA na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani kwa mume mwingine.”

Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa,
10wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe nyumbani kwa watu wako.”

11Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine, ambao wataweza kuwaoa ninyi? 12Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, 13je, mngesubiri mpaka wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa BWANA umekuwa kinyume nami!”

14Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.

15Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”

16Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17Pale utakapofia nami nitafia hapo na papo hapo nitazikwa. BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine cho chote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.

19Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”

20Akawaambia, “Msiniite tena Naomi
1.20 Naomi maana yake Wa Kupendeza, Wa Kufurahisha
, niiteni Mara
1.20 Mara maana yake Chungu
, kwa sababu Mwenyezi
1:20 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania
amenitendea mambo machungu sana.
21Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini BWANA amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? BWANA amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”

22Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabi mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.

Copyright information for Neno