Titus 2

Fundisha Mafundisho Manyofu

Lakini kwa habari yako wewe, inakupasa kufundisha kulingana na mafundisho yenye uzima. Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa unyenyekevu unaostahili utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu ye yote asije akalikufuru neno la Mungu.

Vivyo hivyo, sisitiza vijana wawe na kiasi. Katika kila jambo wewe mwenyewe uwe kielelezo cha matendo mema na katika mafundisho yako uonyeshe unyofu, utaratibu, ukweli na maneno yenye uzima, yale ambayo hayawezi kulaumiwa, hata wale wenye kukupinga watahayari, wakose neno lo lote baya la kusema juu yetu.

Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, 10 wala wasiwaibie, bali watumwa waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwamba kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu kuwa ya kupendeza.

11 Kwa maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya kumcha Mungu, katika ulimwengu huu wa sasa, huku 13 tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo, 14 yeye ndiye aliyejitoa nafsi yake kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na bidii katika kutenda mema.

15 Basi wewe fundisha mambo haya; onya na karipia kwa mamlaka yote. Mtu ye yote asikudharau.

Copyright information for Neno