Zephaniah 2

1Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,
enyi taifa lisilo na aibu,
2kabla ya wakati ulioamuriwa haujafika
na siku ile inayopeperusha kama makapi,
kabla hasira kali ya BWANA haijaja juu yenu,
kabla siku ya ghadhabu ya BWANA
haijaja juu yenu.
3Mtafuteni BWANA, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,
ninyi ambao hufanya lile analoamuru.
Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;
labda mtahifadhiwa
siku ya hasira ya BWANA.

Dhidi Ya Ufilisti

4Gaza utaachwa
na Ashkeloni utaachwa magofu.
Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu
na Ekroni utang'olewa.
5Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,
Enyi Wakerethi;
neno la BWANA liko dhidi yenu,
Ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.
“Mimi nitawaangamiza,
wala hakuna atakayebaki.”
6Nchi kando ya bahari, mahali ambapo wanaishi Wakerethi,
patakuwa mahali pa wachungaji
na mazizi ya kondoo.
7Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,
hapo watapata malisho.
Wakati wa jioni watajilaza chini
katika nyumba za Ashkeloni.
BWANA Mungu wao atawatunza,
naye atawarudishia wafungwa wao.

Dhidi Ya Moabu Na Amoni

8“Nimeyasikia matukano ya Moabu
nazo dhihaka za Waamoni,
ambao waliwatukana watu wangu
na kufanya vitisho dhidi ya nchi yao.
9Hakika, kama niishivyo,”
asema BWANA Mwenye Nguvu Zote,
Mungu wa Israeli,
“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,
Waamori kama Wagomora:
mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,
nchi ya ukiwa milele.
Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;
mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”
10Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,
kwa kutukana na kudhihaki
watu wa BWANA Mwenye Nguvu Zote.
11BWANA atakuwa wa kutisha kwao
wakati atakapoangamiza
miungu yote ya nchi.
Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,
kila moja katika nchi yake.

Dhidi Ya Kushi

12“Ninyi pia, Ee Wakushi,
mtauawa kwa upanga wangu.”

Dhidi Ya Ashuru

13Mungu atanyosha mkono wake dhidi ya kaskazini
na kuangamiza Waashuru,
akiiacha Ninawi ukiwa
na pakame kama jangwa.
14Makundi ya kondoo na ng'ombe yatajilaza pale,
viumbe vya kila aina.
Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba
wataishi juu ya nguzo zake.
Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,
kifusi kitakuwa milangoni,
boriti za mierezi zitaachwa wazi.
15Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha
wakijisikia salama.
Ulisema moyoni mwako,
“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”
Jinsi gani umekuwa gofu,
mahali pa kulala wanyama pori!
Wote wanaopita kando yake wanauzomea
na kutikisa mkono kwa dharau.
Copyright information for Neno