Zephaniah 3

Hatima Ya Yerusalemu

1Ole wa mji wa wadhalimu,
waasi na waliotiwa unajisi!
2Hautii mtu ye yote,
haukubali maonyo.
Haumtumaini BWANA,
haukaribii karibu na Mungu wake.
3Maafisa wake ni simba wangurumao,
watawala wake ni mbwa mwitu wa jioni,
ambao hawabakizi cho chote
kwa ajili ya asubuhi.
4Manabii wake ni wenye kiburi,
ni wadanganyifu.
Makuhani wake hunajisi patakatifu
na kuihalifu sheria.
5BWANA aliye ndani yake ni mwenye haki,
hafanyi kosa.
Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake,
kila kukipambazuka huitimiza,
bali mtu dhalimu hana aibu.
6“Nimeyafutilia mbali mataifa,
ngome zao zimebomolewa.
Nimeziacha barabara ukiwa,
hakuna anayepita humo.
Miji yao imeharibiwa;
hakuna mmoja atakayeachwa:
hakuna hata mmoja.
7Niliuambia huo mji,
‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’
Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali,
wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake.
Lakini walikuwa bado na shauku
kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
8BWANA anasema,
“Kwa hiyo ningojee mimi,
siku nitakayosimama kuteka nyara.
Nimeamua kukusanya mataifa,
kukusanya falme
na kumimina ghadhabu yangu juu yao,
hasira yangu kali yote.
Dunia yote itateketezwa
kwa moto wa wivu wa hasira yangu.
9“Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa,
kwamba wote waweze kuliitia jina la BWANA
na kumtumikia kwa pamoja.
10Kutoka ng'ambo ya mito ya Kushi
watu wangu wanaoniabudu,
watu wangu waliotawanyika,
wataniletea sadaka.
11Siku hiyo hutaaibishwa
kwa ajili ya makosa yote ulionitendea,
kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu
wale wote wanaoshangilia
katika kiburi chao.
Kamwe hutajivuna tena
katika kilima changu kitakatifu.
12Lakini nitakuachia ndani yako
wapole na wanyenyekevu,
ambao wanatumaini jina la BWANA.
13Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;
hawatasema uongo,
wala udanganyifu hautakuwa
katika vinywa vyao.
Watakula na kulala
wala hakuna ye yote
atakayewaogopesha.”
14Imba, Ee Binti Sayuni;
paza sauti, Ee Israeli!
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,
Ee Binti Yerusalemu!
15BWANA amekuondolea adhabu yako,
amewarudisha nyuma adui zako.
BWANA, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;
kamwe hutaogopa tena madhara yo yote.
16Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,
“Usiogope, Ee Sayuni;
usiiache mikono yako ilegee.
17BWANA Mungu wako yu pamoja nawe,
yeye ni mwenye nguvu kuokoa.
Atakufurahia kwa furaha kubwa,
atakutuliza kwa pendo lake,
atakufurahia kwa kuimba.”
18“Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa
nitaziondoa kwenu;
hizo ni mzigo wa fedheha kwenu.
19Katika wakati huo nitawashughulikia
wote waliokudhulumu;
nitaokoa kilema na kukusanya
wale ambao wametawanywa.
Nitawapa sifa na heshima
katika kila nchi ambamo waliaibishwa.
20Wakati huo nitawakusanya;
wakati huo nitawaleta nyumbani.
Nitawapa sifa na heshima
miongoni mwa mataifa yote ya dunia
wakati nitakapowarudishia mateka yenu
mbele ya macho yenu hasa,”
asema BWANA.

Copyright information for Neno