Mwanzo 1

Siku Sita Za Uumbaji Na Sabato

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu Dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu, giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji.

  • Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.
Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi na akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. 11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu. 14 
  • Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe mchana na usiku, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka,
15 nayo iwe ndiyo mianga kwenye nafasi ya anga itoe nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale mchana na usiku, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne. 20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini, kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mkaongezeke mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano. 24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wafugwao kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” 27 

Kwa hiyo Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa kwa ajili ya chakula chenu, 30 cha wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi. Kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

31 Mungu akatazama vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

Habari hati miliki kwa Neno