John 10

Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi. Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje. Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake." Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. 10 Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili. 11 "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. 12 Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya. 13 Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. 14 Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, 15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. 16 Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. 17 "Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. 18 Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."

19 Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. 20 Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?" 21 Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"

22 Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. 23 Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. 24 Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi." 25 Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. 26 Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. 28 Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. 29 Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. 30 Mimi na Baba, tu mmoja." 31 Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. 32 Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?" 33 Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu." 34 Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: Mimi nimesema, ninyi ni miungu? 35 Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. 36 Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: Unakufuru, eti kwa sababu nilisema: Mimi ni Mwana wa Mungu? 37 Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini. 38 Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."

39 Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. 40 Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. 41 Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa." 42 Watu wengi mahali hapo wakamwamini.

Copyright information for Swahili