Matthew 14

Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake." Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!" Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji." Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. 10 Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. 11 Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. 12 Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.

13 Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. 14 Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. 15 Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula." 16 Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula." 17 Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili." 18 Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa." 19 Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. 20 Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21 Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.

22 Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng'ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu. 23 Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, 24 na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. 25 Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu. 27 Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!" 28 Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako." 29 Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. 30 Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!" 31 Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?" 32 Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. 33 Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."

34 Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. 35 Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, 36 wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.

Copyright information for Swahili