Romans 10

Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu. Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi." Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: Nani atapanda mpaka mbinguni? (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: Nani atashuka mpaka Kuzimu (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)." Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka. 10 Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa. 11 Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika."

12 Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. 13 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa." 14 Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? 15 Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!" 16 Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?" 17 Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. 18 Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu." 19 Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu." 20 Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu." 21 Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii."

Copyright information for Swahili