2 Chronicles 25

Amazia Mfalme Wa Yuda

(2 Wafalme 14:2-20)

1 aAmazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani kutoka Yerusalemu. 2 bAkatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, lakini sio kwa moyo wake wote. 3 cBaada ya ufalme kuimarika mikononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. 4 dHata hivyo hakuwaua watoto wao, lakini akafanya sawasawa na ilivyoandikwa katika Sheria, katika Kitabu cha Mose, ambako Bwana aliamuru: “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

5 eAmazia akawaita watu wa Yuda pamoja, akawaweka chini ya majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia kufuatana na jamaa zao katika Yuda yote na Benyamini. Kisha akawahesabu wale wenye umri wa miaka ishirini au zaidi na akakuta kwamba walikuwa wanaume 300,000 watu walio tayari kwa utumishi wa jeshi, walio na uwezo wa kutumia mkuki na ngao. 6Akawaajiri pia watu 100,000 wapiganaji kutoka Israeli kwa talanta 100 za fedha.
Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75.


7 gLakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe kwa kuwa Bwana hayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na yeyote wa watu wa Efraimu. 8 hHata kama ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.”

9 iAmazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta 100 za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?”

Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwana aweza kukupa zaidi sana ya hizo.”

10Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.

11 jNdipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake kwenye Bonde la Chumvi, ambako aliua watu 10,000 wa Seiri. 12 kJeshi la Yuda pia likawateka watu 10,000 wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu hata wote wakavunjika vipande vipande.

13Wakati huo yale majeshi Amazia aliyoyarudisha na ambayo hakuyaruhusu kushiriki katika vita, yalivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Yakawaua watu 3,000 na kuchukua kiasi kikubwa sana cha mateka.

14 lAmazia aliporudi kutoka kuwachinja Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea kafara za kuteketezwa. 15 mHasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”

16 nWakati nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza, ya nini uuawe?”

Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza shauri langu.”

17 oBaada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”

18 pLakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. 19 qWewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini utafute matatizo na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”

20 rHata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu. 21Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. 22Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. 23 sYehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400.
Dhiraa 400 ni sawa na mita 180.
24 uAkachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.

25 vAmazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. 26Kwa habari ya matukio mengine katika utawala wa Amazia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na wa Israeli? 27 wKuanzia wakati ule Amazia alipogeuka na kuacha kumfuata Bwana walifanya shauri baya dhidi yake huko Yerusalemu naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi nao wakamuulia huko. 28 xAkarudishwa kwa farasi na akazikwa pamoja na baba zake katika Mji wa Yuda.

Copyright information for SwhNEN