2 Kings 10:1-14
Jamii Ya Ahabu Yauawa
1 aWakati huu katika Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema, 2“Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha, 3mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke juu ya kiti cha enzi cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.”4Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?”
5 bBasi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.”
6Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.”
Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea. 7 cHiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli. 8Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.”
Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji mpaka asubuhi.”
9Asubuhi yake, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyefanya shauri baya dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa? 10 dFahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo Bwana amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. Bwana amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Eliya.” 11Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike.
12Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani, Beth-Ekedi ya wachunga kondoo, 13 eYehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?”
Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.”
14 fYehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.
Copyright information for
SwhNEN