2 Kings 20:12-19
Wajumbe Kutoka Babeli
(Isaya 39:1-8)
12Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. 13Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.14Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
15Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”
16Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana: 17 aHakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. 18 bNao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
19Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
Copyright information for
SwhNEN